WENYE CHANGAMOTO ZA AFYA YA AKILI WAJE, SASA TUNA HICHO KITENGO – DKT. MASENGA
Posted on: February 25th, 2025
Wananchi wenye changamoto na magonjwa ya Afya ya Akili, wenye ndugu na wenye kuhitaji ushauri, wamehusiwa kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe ili kukutana na wataalamu amabao watasaidia kuwapatia ushauri, matibabu ya dawa na saikolojia kutokana na changamoto wanazopitia.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Mtaalamu wa magonjwa hayo, Dkt. Shomari Kapombe katika Kipindi cha Afya Kwanza kinachorushwa Kings FM Radio.
Amesema kuwa kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, yaliyoonesha Tanzania ina watanzania Milioni 60 kati ya hao Milioni 7 wana matatizo ya Afya ya Akili.
Ameeleza kuwa miongoni mwa magonjwa ya Afya ya Akili yanayoonekana kuwa ya kujirudia mara kwa mara kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe ni hali ya kuwa na Hofu pamoja na Msongo wa Mawazo.
“Ukifika Hospitali utakutana na watu wa mapokezi waeleze kuwa unahitaji kuonana na Daktari wa Magonjwa ya Afya ya AKili watakuelekeza utakuja chumba namba 15 kupata hiyo huduma” amesema
Ameitahadharisha jamii kuacha Imani potofu dhidi ya watu wenye changamoto na Magonjwa ya Afya ya Akili badala yake wawapeleke katika vituo vya afya vya kutolea huduma, huku akiiasa pia kuepuka kuwaita majina yasiyofaa
“Jamii itambue kuwa Magonjwa ya Afya ya Akili yanaweza kumkumba mtu yeyote, hivyo tusiwatenge watu wenye changamoto hizi wala tusiwaone tukawaita majina ya ajabu; tunakuwa hatuwasaidii na badala yake tunatengeneza hali ya kuwanyanyapaa. Tuwapende na tuwahudumie kwa sababu hata sisi tunaweza kukumbwa na hali hii kutokana na maisha tunayoishi” amemalizia Dkt. Masenga.