Contact Us | FAQ | Mails | Complaints |

UJIO WA MUUGUZI MKUU WA SERIKALI NJOMBE RRH, ASISITIZA UBORA WA HUDUMA

Posted on: May 31st, 2024

Muuguzi Mkuu wa serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga Tanzania Bi. Ziada Sellah, jana Mei 31(jioni) amefanya ziara katika 

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, ambapo aliweza kuzungumza na wauguzi, wakunga na wahudumu wa Afya (Medical Attendants) kwa lengo

 la kukumbusha mambo muhimu ambayo makundi hayo yanatakiwa kuzingatia katika muda wote wanapokuwa katika utumishi wa Umma.


Miongoni mwa maeneo aliyotilia mkazo katika mazungumzo na watumishi hao, ni pamoja na kufanya Tafiti mbalimbali zinazohusu

 masuala ya Afya, ambapo alisisitiza tafiti hizo lazima ziambatane na Ubunifu ili kuzifanya kazi zao kuwa na tija katika uboreshaji wa

 Huduma za Afya, huku akiwaasa pia kujiendeleza kielimu.


“Jamani twendeni tukasome; uuguzi unabadilika kila wakati. Lazima tujiendeleze ili tuendane na wakati tulionao katika kuwahudumia wananchi; 

Hii ndio kazi tuliyoisomea lazima tuipende na tujivunie kuwa wauguzi” amenukuliwa.

Bi. Sellah alisisitiza pia Maadili ya Utumishi kwa Umma, kwa kuhakikisha wanazingatia muda wa kuingia na kutoka kazini, kuvaa sare kazini, kuzingatia miongozo

, sheria na taratibu za kumhudumia mgonjwa, lugha ya staha kwa wateja inayoleta mawasiliano mazuri baina ya Muuguzi na Mteja wake, pamoja na kutunza taarifa za maendeleo ya Mgonjwa.


“Niendelee kuwasisitiza kuwa tuzingatie Maadili ya kazi zetu, tusitamani kupelekwa kwenye Baraza la Uuguzi na Ukunga, kwa kukiuka taratibu na 

miongozo ya Utoaji huduma zilizo bora. Mhe. Waziri wa Afya amekuwa akisisitiza suala hili; hivyo ni lazima tuhakikishe tunafuata pia miongozo ya 

Wizara ya Afya ikiwemo kuzingatia haki na wajibu wa mtoa huduma, pamoja na haki na wajibu wa anayehudumiwa (mgonjwa).


Alimalizia kikao hicho kwa kuwaasa wauguzi na wakunga kutunza taarifa za matibabu ya Mgonjwa kwa ajili ya rejea pindi inapotokea shida au 

hali ya sintofahamu pahala pakazi.

Awali akitoa taarifa ya Uuguzi, ukunga, Ustawi wa Jamii na Lishe, Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe Bi. Clever Mustapha, 

alitaja baadhi ya mafanikio ya Idara hiyo kuwa ni pamoja na kufanikiwa kupata watumishi wa ajira mpya wahudumu wa afya 3 na Afisa lishe 1, 

kufanya usimamizi shirikishi Idara ya Uuguzi na Ukunga kwa robo ya tatu Jan- Machi 2024,


Mafanikio mengine yaliyotajwa ni pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa wa msamaha wapatao 91 kuanzia Jan- Apr 2024 ikiwa ni chakula pamoja

 na matibabu, kufanikiwa kupunguza misamaha kutoka asilimia 2.56% hadi 0.86% sawa na fedha za kitanzania 1,367,490/= hadi 699,000/= kwa miezi 

mitatu, pamoja na kufanikiwa kuanza mchakato wa kupata wanafunzi tarajali (intern nurses).


 Pia alipata wasaa wa kueleza baadhi ya Changamoto zinazoikumba Idara hiyo kuwa ni pamoja na Uhaba wa watumishi waliopo bado hawatoshelezi 

kutokana na ongezeko la huduma kama vyumba vya upasuaji na usimamizi kwa wanafunzi (clinical instructors), kitengo cha lishe bado hakijaanzishwa

 mtaalamu tuliyepata ana changamoto za kiutumishi bado hajaripoti, kutokuwa na huduma bobezi za Uuguzi na Ukunga kama critical care, 

midwifwery na neonate.


Wakati huo, Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Njombe Bi. Sophia Mfungati ameiomba serikali kuendelea kutoa nafasi za ufadhili wa 

masomo na kutoa kipaumbele kwa mkoa wa Njombe kwa wauguzi ikiwemo katika eneo la Uuguzi Bingwa ambapo mpaka sasa

 mkoa wa Njombe unao wauguzi wawili tu, katika ngazi hiyo.