UHAMIAJI WAADHIMISHA KILELE CHA SIKU YA UHAMIAJI DUNIANI KWA KUTOA MISAADA NA KUFANYA USAFI, NJOMBE RRH
Posted on: December 18th, 2024Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Njombe limeadhimisha siku ya wahamiaji Duniani, ambayo hufanyika kila tarehe 18, Desemba kwa kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, ambapo ziara yao iliambatana na kufanya usafi eneo la Hospitali, na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa wanaoendelea kupata huduma, hasa katika Jengo la Huduma za Afya ya Mama na Mtoto.
Akizungumza baada ya shughuli hiyo, Mratibu Mwandamizi, Etinesi Crymont Msowela ambaye ni Naibu Afisa Uhamiaji Mkoa wa Njombe, amesema kuwa ujio wao ni sehemu ya Maelekezo kutoka makao makuu ya Jeshi hilo, ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli za usafi, kuwasaidia wahitaji na kutoa misaada katika maeneo mbalimbali ikiwemo Hospitali.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi, Dkt. Lazaro Jassely ameushukuru Uongozi wa Uhamiaji kwa kuthamini na kuona umuhimu wa kuja kutembelea katika Hospitali ya Rufaa kwa kutoa misaada na usafi, hivyo akaasa jamii kuiga na kuendelea kujitokeza kushiriki shughuli mbalimbali zinazohusu ujenzi wa Taasisi hii.