TUME YA NGUVU ZA ATOMIKI YAFANYA UHAKIKI WA UBORA WA HUDUMA ZA MIONZI NJOMBE RRH
Posted on: December 19th, 2024Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) imefanya ziara ya ukaguzi na Uhakiki wa Ubora wa Huduma za Radiolojia Mkoani Njombe kwa kutembelea vituo vipatavyo 32 ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Akizungumza jana Desemba 18 baada ya kukamilisha zoezi hilo, Mkuu wa Kanda ya Kati, Bw. Machibya Matulanya ameridhishwa na ubora huduma za Radiolojia kwa vituo vilivyopo Nyanda za Juu Kusini, ikijumuisha mikoa ya Njombe, Iringa, pamoja na Ruvuma.
"Kwa zaidi ya asilimia 80 ya vituo tulivyotembelea katika Ukanda huu vimekidhi mahitaji ya kitaifa ya usalama wa mionzi na asilimia 20 ya vituo tulivyopitia vimekuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji marekebisho ya haraka." Amesema Bw. Matulanya.
Miongoni mwa maeneo yaliyoainishwa kufanyiwa ukaguzi Mkoani Njombe yalihusisha ukaguzi wa Mashine za X - Ray za kawaida, X - Ray za Kinywa na Meno, Mashine za CT Scan, MRI, na mashine za Viwandani.
Ametoa wito kwa mafundi sanifu wa vifaa vya Atomiki kuwa na leseni kwa kuzingatia sheria ya nguvu za atomiki kifungu cha 25.
Ameasa pia taasisi zinazonunua vifaa vipya vyenye nguvu ya Atomiki kuhakikisha vinasajiliwa, na kukaguliwa, pamoja na kupewa leseni kabla ya kuanza kutumika.
Mratibu wa Huduma za Radiolojia Mkoa wa Njombe, Bi. Eva Nathaniel Sijaona, ameomba serikali kuendelea kuajiri watumishi katika huduma mionzi ili maeneo yaliyopata vifaa hivyo yaweze kutumika na kuwahudumia wananchi katika maeneo yao.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Dkt. Lazaro Jassely ameahidi kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe kupitia wataalamu wake, itaendelea kuwajengea uwezo wataalamu walio katika vituo vilivyopo chini yake, ikijumuisha Hospitali za Halmashauri, Wilaya na vituo vya Afya.