Contact Us | FAQ | Mails | Complaints |

TANROADS - NJOMBE WAADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KWA KUTOA MAHITAJI NJOMBE RRH

Posted on: July 5th, 2024

Watumishi kutoka Ofisi ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) mkoa wa Njombe wameadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutoa mahitaji mbalimbali katika Jengo la Huduma za Mama na Mtoto, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe leo Julai 5, 2024 na kuwajulia hali wanawake wanaotarajia kujifungua, waliojifungua na waoauguza watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Akizungumza baada ya kutoa mahitaji hayo Kaimu Afisa Rasilimali watu, TANROADS Njombe, Bi. Monica Mwaimu amesema kuwa ujio wao katika Jengo la Huduma za Mama na Mtoto ni kutambua nafasi yao kama watumishi wa Umma kwa kuamua kuadhimisha siku yao kwa kutoa misaada mbalimbali.

“Mimi na wenzangu kwa kutambua umuhimu wa maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma, tumeamua kuja kutoa mahitaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe hasa kwa Jengo la Huduma za Mama na Mtoto,tukiamini mahitaji haya yatawasaidia kwa kipindi watakachokuwa hapa Hospitali wakipatiwa huduma” amesema Bi. Mwaimu.

Naye Muuguzi Msimamizi wa Huduma za Afya ya Mama na Mtoto, Ramadhan Ramadhan akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa Idara hiyo amesema kuwa “Tunapenda kuwashukuru sana ndugu zetu kutoka TANROADS hasa kwa kuja na kuwapa faraja ndugu zetu wanaohudumiwa hapa.

Lakini,tunafahamu kuwa TANROADS ni jirani zetu, hivyo kwa kutambua ukaribu wet una kutoa misaada hii inafungua njia nyingine ya kuongeza zaidi ushirikiano baina ya Taasisi hizi mbili za serikali.” Amenukuliwa Ramadhani Ramadhani.

Naye Mkuu wa Idara ya Huduma za Watoto Dkt. Jovitha Mtenga ameshukuru Taasisi ya TANROADS – Njombe kwa misaada hiyo, akisisitiza waendelee kufanya hivyo kwa kuwa inaongeza hali ya kujenga utu na kupata baraka zaidi.