Contact Us | FAQ | Mails | Complaints |

NJOMBE RRH YAPOKEA WATUMISHI 80, AJIRA MPYA

Posted on: January 3rd, 2025

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe imetoa mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wapya wapatao 80, lengo likiwa ni kuwaelekeza kanuni, taratibu, miongozo mahali pa kazi, pamoja na utoaji wa huduma bora katika maeneo yao ya kazi.


Mafunzo hayo yaliyofunguliwa tarehe 30, Desemba 2024 na kufungwa Januari 2, 2025 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Dkt. Gilbert Kwesi, yamewanufaisha watumishi hao katika maeneo mbalimbali ikiwemo Haki na wajibu wa Mtumishi wa Umma, Kanuni za Utendaji kazi kwa Mtumishi wa Umma, Muundo wa  Uendeshaji wa Hospitali, na Uzuiaji Maambukizi mahali pa kazi.

 

Awali akifungua mafunzo hayo Dkt. Kwesi aligusa maeneo mbalimbali ambayo watumishi hao walipaswa kuyatilia maanani hasa katika kukamilisha maana halisi ya Mtumishi wa Umma. "Lazima kama Mtumishi wa Umma ujue sheria, kanuni na mipaka yako mahali pa kazi ili kujiepusha na matatizo yanayoweza kukupata ukiwa katika utekelezaji wa majukumu yako. Ifahamike kuwa kutojua sheria haikupi nafasi ya kuvunja sheria, hivyo lazima tuhakikishe tunafuata miiko na maadili ya Utumishi wa Umma" Alisema Dkt. Kwesi


Naye Mratibu wa Mafunzo na Utafiti, Bw. Evaristus Makota, amewashukuru watumishi wote waliohudhuria mafunzo hayo kwa kuwa na utayari wa kujifunza kwa muda huo wa siku tatu, huku akitoa ujumbe wa kuyafanyia kazi yale yote waliyojifunza. 


Watumishi hao wamenufaika pia na mafunzo mbalimbali ikiwemo namna ya kukabiliana na kujiepusha na rushwa kupitia TAKUKURU, pamoja na kula kiapo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Isack Romanus Mlowe  mbali na kiapo hicho, aliwaasa Madaktari kuwa makini katika kuandika ripoti zinazohitaji ushahidi wa kimahakama.


Maeneo mengine waliyonufaika katika mafunzo nayo ni pamoja na Elimu kuhusu Usimamizi wa fedha, Manunuzi na  Ugavi, Huduma bora kwa Mteja, Mfumo unaohakikisha Usalama mahali pa kazi (5S) Mifumo ya uagizaji dawa katika Bohari ya Dawa ya Hospitali, Ujuzi kuhusu Maisha, na namna ya kufaidika na mfuko wa Akiba na Mikopo - Njombe RRH SACCOS.


 Miongoni mwa waliokuwa wawezeshaji mafunzo hayo ni pamoja na Bw. Jafary Simika, Afisa Utumishi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Akoheki Mbapila kutoka TAKUKURU,Samwel Gidaguda, Afisa Usalama, Monica Mtata - Mtunza Kumbukumbu.


Wengine ni pamoja na Handhuruni Saburi,Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ugavi -Njombe RRH, Rehema Nyongole, Afisa Afya Kinga na Mazingira - Njombe RRH,  Evaristus Makota Mratibu wa Mafunzo na Utafiti - Njombe RRH, Irene Lazaro, Mfamasia - Njombe RRH , Paschal Ndugali, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu - Njombe RRH, Ashery Mwalukolo, Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora wa Huduma kwa Mteja na Rasuli Chihako, Afisa Fiziotherapia, na Mratibu wa Michezo - Njombe RRH.