Contact Us | FAQ | Mails | Complaints |

NJOMBE RRH YAADHIMISHA SIKU YA WATOTO WALIOZALIWA KABLA YA WAKATI

Posted on: November 17th, 2024

Ili kuepukana na tatizo la Watoto kuzaliwa kabla ya wakati, pamoja na kuzaliwa na uzito pungufu; jamii imeaswa kuzingatia mtindo bora wa Maisha ikiwemo lishe bora, kuachana na uvutaji wa sigara kwa wajawazito au mwanaume anayeishi na mjamzito, na kuacha matumizi holela ya dawa na matumizi ya dawa za kienyeji zisizothibitishwa.


Wito huo umetolewa leo Novemba 18, 2024 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Dkt. Gilbert Kwesi, aliyekuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Watoto waliozaliwa kabla ya wakati  ( Pre – Mature Day) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.

Ujumbe wa Dkt. Kwesi umeambatana na kuendelea kuikumbusha Jamii ya Mkoa wa Njombe kutumia fursa ya uwepo wa vyakula mbalimbali vya nafaka na matunda vinavyopatikana mkoani hapa ili kuondokana na tatizo la Udumavu.


Amesema “Bahati nzuri Mkoa huu Mungu ametujalia tuna vyakula vingi na hali ya hewa nzuri inayoweza kustawisha mazao; niwaombe wananchi wa mkoa wa Njombe tutumie uwepo wa fursa hii ya uwepo wa vyakula ili vinufaisha afya zetu ili tuepukane na tatizo la Udumavu”


Amesisitiza Idara ya Magonjwa ya Wanawake na Uzazi kuendelea kushirikiana na Idara ya Watoto kutoa elimu kupitia Huduma Mkoba (Outreach) kuwa na mikakati ya pamoja ya kutoa elimu kuhusiana na matatizo yanayweza kupelekea tatizo la kujifungua kabla ya wakati au kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu ikiwemo kuvuta sigara, unywaji wa pombe na matumizi holela ya dawa.


“Miongoni mwa matatizo yanayochangia ni pamoja na Mimba za mtoto zaidi ya mmoja, matatizo kwenye mfuko wa uzazi; hivyo lazima tutoe elimu hii ili wanawake wote waliofikiwa na elimu hiyo iwasaidie kupata uzazi ulio salama” amesema Dkt. Kwesi.


 Miongoni mwa zilizoelezwa kama changamoto na Mkuu wa Idara ya Watoto, Dkt. Mariam Gaitani ni upungufu wa Wauguzi, ambapo Mganga Mfawidhi ameagiza Muuguzi Mfawidhi kuwapeleka wauguzi katika Idara hiyo, baada ya serikali kuleta wauguzi wapya wapatao Arobaini (40) kwa ajira zilizotolewa hivi karibuni.


Pia ameagiza uwepo wa mafunzo ya kujengeana uwezo katika Idara yafanyike mara kwa mara kupitia Uratibu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rasilimali watu, huku akiwaasa wauguzi kujiendeleza kielimu ili kupata wauguzi Mabingwa.


Naye Mkuu wa Idara ya Watoto amewaasa wanawake kuchukua juhudi za makusudi pindi tu wanapojiandaa kubeba ujauzito au wanapogundua dalili za awali za ujeuzito kwa kuanza kuhudhuria Kliniki mapema, kuzingatia maelekezo atakayopewa na mtaalamu wa afya, ikiwemo matibabu ya magonjwa ya kuambukiza; amesisitiza lishe bora kwa rika balehe, kutotumia dawa za asili zisizothibitishwa, na kuacha matumizi ya dawa za kulevya.


Dkt. Gaitani ameiasa pia jamii kushiriki kikamilifu pindi inapopata mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati au mwenye uzito pungufu kwa kumpa kumbato la Ngozi kwa Ngozi kifuani (Kangaroo Mother Care -KMC) kwa kile alichoeleza tafiti zimeonesha hali hiyo inasaidia katika kupunguza vifo vya Watoto hao waliozaliwa kabla ya wakati.

 Siku ya Mtoto njiti kwa Mwaka huu 2024, imebebwa ba Kaulimbiu isemayo “Kitendo Kidogo Matokeo Makubwa, Mtoto Njiti Anaishi, Apendwe Sana Athaminiwe"