MKURUGENZI WA HUDUMA ZA TIBA AKAGUA UTOAJI HUDUMA, NJOMBE RRH
Posted on: October 30th, 2024Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea mapema leo Oktoba 30, ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe ambapo amekagua utoaji huduma katika maeneo mbalimbali ya Hospitali na kuridhishwa na huduma zinazotolewa.
“Nimefurahia kuona mazingira ni masafi, mashuka yametandikwa vizuri, kutokana na uwepo wa baridi mablanketi yapo ya kutosha na safi, na wagonjwa wote niliowahoji hakuna mgonjwa ambaye amelalamika. Jambo hili ni zuri na mnapaswa kuliendeleza” Amesema Dkt. Nyembea.
Akiwa ameambatana na Kaimu Mganga Mfawidhi, Dkt. Barnaba Baraka Mgonja, na Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Hospitali (RRHMT) katika ukaguzi huo Mkurugenzi ametembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Mapokezi, Vipimo vya Awali, Huduma za Dawa (Famasi) Jengo la Huduma za Mama na Mtoto, Maabara, Huduma za Upasuaji, Huduma za Dharura na wagonjwa Mahututi, Utengamao na Huduma za Uchunguzi wa mfumo wa Chakula (Endoscopy).
Baada ya kukagua maeneo hayo amepokea Taarifa ya Hospitali ambapo taarifa hiyo iliangazia maeneo mbalimbali ikiwemo huduma zinazotolewa, hali ya uwepo wa watumishi, hali ya utoaji huduma, upatikanaji wa Dawa, Utekelezaji wa programu ya usafi wa Mazingira, Huduma ya Damu Salama, Utekelezajiwa Afua za Lishe, na Uchangiaji wa Huduma za Afya.
Pia taarifa hiyo imejikita katika mafanikio ya Hospitali ambayo yamejumuisha Kuongezeka kwa majengo ya kutolea huduma kutoka jengo moja mwaka 2019 hadi majengo 12, mwaka 2024, kuajiri watumishi 53 wa kada mbalimbali za Afya kwa njia ya Mkataba, kupata mashine ya kuchunguza na kutibu magonjwa ya mfumo wa chakula ( endoscopy ) na Vifaa tiba kwa ajili ya kitengo cha Huduma ya vifaa saidizi/ bandia ( prosthetic and orthotics )
Mafanikio mengine yaliyoelezwa mbele ya Mkurugenzi ni kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya vyanzo vilivyopo kwa zaidi ya asilimia 100, pia kiwango cha upatikanaji wa dawa muhimu kimeongezeka kutoka asilimia 95.6 mwaka 2023 hadi 97 kwa mwaka 2024.
Upande wa Changamoto zilizoainishwa mbele ya Mkurugenzi ni pamoja na upungufu wa rasilimali watu kwa asilimia 65 kwenye kada mbalimbali, kukosekana kwa usafiri wa uhakika kwa watumishi wanaotoka umbali wa zaidi ya kilomita 20, kutopokuwepo kwa njia ya umeme kwa matumizi ya Hospitali pekee, ukosefu wa Uzio kwa ajili ya ulinzi wa eneo la Hospitali, upungufu wa miundombinu ya kutolea huduma kama jengo la upasuaji na utawala.
Mkurugenzi ameahidi kuwa Wizara ya Afya itahakikisha inaongeza wataalamu mbalimbali ili kupunguza uhaba uliopo, kuipatia Hospitali gari kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uendeshaji wa Huduma za Afya, pamoja na kuhakikisha inawasiliana na uongozi wa Mkoa ili kutatua shida ya kukosekana kwa njia maalumu ya Umeme katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Ametoa wito kwa Uongozi wa Hospitali kuhakikisha mazingira rafiki ya kutoa huduma, kuweka wazi mfumo wa ukusanyaji maoni ikiwemo kutengeneza makundi Sogozi ya WhatsApp na kutembelea maeneo ya Hospitakli yenye Mkusanyiko wa watu kwa ajili ya kusikiliza kero na kuzitatua.
Amesisitiza wataalamu wa Afya kuwahudumia wagonjwa kwa muda ili kupunguza malalamiko ya watu.