Contact Us | FAQ | Mails | Complaints |

WANANCHI 1756 WAHUDUMIWA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA NA BOBEZI, NJOMBE RRH

Posted on: December 5th, 2024

Jumla ya wananchi wapatao 1756 wamepatiwa matibabu katika Kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi waliohudumu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe huku kati yao 94 wakifanyiwa upasuaji kwa siku tano (Desemba 2 - Desemba 6)

Hayo yameelezwa jana Desemba 6 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Dkt. Gilbert Kwesi, ambaye ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwezesha kufanyika kwa kambi hiyo.

Ametoa shukrani kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Mganga Mkuu wa Mkoa kuwa sehemu ya uwezeshaji wa zoezi hilo, Wadau mbalimbali wakiwemo USAID Afya Yangu Nyanda za Juu Kusini, Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mgao, Benki ya CRDB, na vyombo vya habari kuwa sehemu ya watu waliofanya zoezi hilo kuwa na ufanisi.

Pia Dkt. Kwesi ametoa shukrani kwa Waganga wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa ikiwemo Amana, Mbeya, Songwe, na Songea, Hospitali za Kanda za Mbeya, na Benjamin Mkapa, Taasisi ya Ocean Road na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kutoa wataalamu mbalimbali wakiwemo Mabingwa Bobezi kwenye maeneo mbalimbali ambao kwa sehemu kubwa wamesaidia katika kutatua changamoto mbalimbali za kiafya kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe.

Ameendelea kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe kuendelea kutumia huduma za Kibingwa zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, na zile ambazo hazitokuwepo ameahidi kuendeleza utaratibu wa kuwa na Kliniki Maalumu za Mabingwa na Bingwa Bobezi kwa maeneo yenye uhitaji mkubwa ambayo Hospitali haijafanikiwa kuwa nayo.