Contact Us | FAQ | Mails | Complaints |

KATIBU TAWALA MKOA WA NJOMBE AZUNGUMZA NA MENEJIMENTI YA NJOMBE RRH

Posted on: July 4th, 2024

Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omari amekutana na Timu ya Menejimenti ya Uendeshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe (RRHMT) leo Julai 4 na kupata taarifa ya hali ya utoaji huduma, uendeshaji na ushughuliakiaji wa changamoto mbalimbali zilizoonekana kipindi cha nyuma ambapo katika ujio wake ameambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dkt. Juma Mfanga.


Miongoni mwa yaliyoelezwa katika taarifa kwa Katibu Tawala iliyosomwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Dkt. Gilbert Kwesi, ni pamoja na Huduma zinazotolewa, Hali ya uwepo wa Watumishi, Hali ya Upatikanaji wa Dawa na Vifaa Tiba, Hali ya utoaji huduma kuanzia Januari 2024 – Juni 2024.


Pia taarifa hiyo ilihusisha hali ya Uchangiaji wa huduma za Afya, Mafanikio, changamoto, mikakati ya Hospitali, pamoja na Mapendekezo.


Akisoma taarifa hiyo kwa niaba ya RRHMT Mganga Mfawidhi, Dkt. Kwesi ameeleza uwepo wa maboresho yaliyoleta mafanikio katika utoaji huduma ikiwemo ongezeko la hali ya upatikanaji wa Dawa kutoka asilimia 95.6 hadi 97 kwa mwaka 2024, kuajiri watumishi 52 wa kada mbalimbali za Afya kwa njia ya Mkataba, kukamilisha ukarabati wa vyumba vya upasuaji jengo la wazazi, kuhuishwa kwa kamati mbalimbali za Hospitali, pamoja na ununuzi wa mashine ya Endoscopy itakayosaidia kufanya vipimo na baadhi ya matibabu katika mfumo wa chakula.


Kati ya changamoto zilizoibuliwa katika taarifa hiyo ni upungufu wa Rasilimali watu kwa asilimia 47.6 kwa kada mbalimbali, kutokuwepo kwa njia ya umeme kwa matumizi ya Hospitali pekee yake, hali inayopelekea gharama kubwa za ununuzi wa mafuta pindi umeme unapokatwa, upungufu wa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na kufanya upanuzi wa majengo ya kutolea huduma, na kukosekana kwa usafiri wa uhakika kwa watumishi.


Akizungumza na Menejimenti ya Hospitali, Katibu Tawala Bi. Judica Omari alitumia wasaa huo kutolea ufafanuzi kwa baadhi ya changamoto zilizoelezwa na RRHMT kupitia taarifa iliyotolewa mbele yake, ambapo ametoa ushauri, na baadhi ya mapendekezo katika changamoto hizo.


Miongoni mwa yaliyotolewa njia za kutatua ni pamoja na kuahidi watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe waliokuwa wamepelekwa katika vituo vya Halmashauri mbalimbali za mkoa kurudishwa kituoni, ameshauri kufanya tathmini na kukutana na wadau wa Nishati ya Jua ili kuona namna ya kuwa na umeme utokanao na jua ili kupunguza gharama kubwa ya ununuzi wa mafuta pindi umeme unapokatwa pamoja na kuanzisha program ya uvunaji maji kipindi cha masika ili kupunguza gharama za bili ya maji.


Ametoa ushauri kwa menejimenti kutoa nafasi ya ushiriki na uwazi kwa watumishi katika vikao, vitengo na idara zao, pia watumishi kutoa ushirikiano kwa Menejimenti na Mganga Mfawidhi ili kuwa na maendeleo yanayotokana na nguvu ya pamoja.

Katibu Tawala amemaliza kwa kuwaasa Menejimenti ya Hospitali kuendelea kuwasimamia watumishi kufuata miongozo, taratibu za utumishi wa Umma ikiwemo kufika kazini kwa wakati na kuepukana na utoro mahali pa kazi.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Juma Mfanga, amepongeza uwepo wa mabadiliko chanya katika utoaji huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe

“Nawapongeza sana kwa mabadiliko makubwa, ukilinganisha na huko nyuma, hata simu za malalamiko zimepungua. Niwasishi kuendelea kufuata sheria, taratibu na miongozo ya kutoa matibabu iliyowekwa, tukiendelea kufanya kazi kwa kushirikiana” amesema Dkt. Mfanga.