Contact Us | FAQ | Mails | Complaints |

KATIBU TAWALA AZINDUA BODI YA USHAURI YA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA NJOMBE

Posted on: January 22nd, 2025

Katibu Tawala, Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omari amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka leo Januari 23, 2025 katika hafla ya Uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe yenye Jumla ya wajumbe 9.


Bi. Judica, ameitaka Bodi hiyo kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya Afya mkoani Njombe kwa kipindi cha Miaka mitatu ambacho itakuwa ikifanya kazi, hasa katika kuhakikisha inasimamia ubora wa huduma, kuibua miradi ya maendeleo, na kushirikiana na Uongozi wa Hospitali katika Utekelezaji wa mipango mbalimbali.


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali Balozi Danford Mpumilwa, ameahidi kuwa Bodi hiyo itakwenda kuwa chachu ya maendeleo makubwa yatakayoshuhudiwa kwa kipindi cha miaka mitatu ambacho Bodi hiyo itakuwa katika majukumu yake.


“Tuwajibike na kuifanya Hospitali hii kuwa ya mfano hapa nchini; kwa kutoa mawazo chanya yatakayosaidia katika ujenzi wa Taasisi hii” amesema.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi, Dkt. Gilbert Kwesi ambaye ni Katibu wa Bodi hiyo amesema kuwa ushirikiano na kuwa na nia moja ndiyo chachu kubwa itakayoleta mapinduzi yanayotarajiwa kupitia Bodi hiyo.

Dkt. Kwesi, amewashukuru wawezeshaji wa mafunzo, wajumbe wa Bodi na Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Hospitali kwa ushiriki wao mzuri kuanzia siku ya kwanza ya mafunzo hadi siku ya Uzinduzi.


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Juma Mfanga, ametumia Jukwaa hilo kwa kuhamasisha Bodi kuwa sehemu ya Uhamasishaji wa Vita dhidi ya Udumavu.


Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ambao wameteuliwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wamenufaika na kujengewa uwezo kuhusu namna Bodi hiyo inavyotakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana na Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Hospitali (RRHMT), Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Afya Mkoa (RHMT), Katibu Tawala Msaidizi (Mganga Mkuu wa Mkoa) na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya kwa utangulizi wa mafunzo yaliyofanyika hapo jana Januari 22.


Miongoni mwa maeneo ambayo wamejengewa Uwezo ni pamoja na kufahamu kwa historia namna sekta ya Afya ilivyokuwea ikifanya kazi kabla ya uhuru, baada na hata sasa,kuuufahamu muundo wa uendeshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, majukumu na wajibu wa Bodi, mahusiano na mtitiriko wa mawasiliano kati ya Bodi, Katibu Tawala na Wizara ya Afya.


Pia Bodi imewezeshwa kuyafahamu majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukusanya mawazo na mahitaji ya huduma ya jamii na kuyawasilisha, kuyajadili na kuyaingiza kwenye mpango wa utekelezaji wa Hospitali, uangalizi wa mali na samani za Hospitali, kuraghabisha na kuhamasiaha wadau kuchangia katika ujenzi wa miradi na uboreshaji wa huduma za Hospitali, kushiriki, kuandaa na kupitisha mpango kabambe wa Hospitali (CHOP), kuwahabarisha/kuwaelimisha wafanyakazi kuhusu masharti ya kazi/huduma, mipango ya motisha na maendeleo ya wafanyakazi.


Wajumbe wa Bodi ya Ushauri wamepata wasaa wa kutembelea maeneo mbalimbali ya Hospitali kwa ajili ya kushuhudia namna huduma za Afya zinavyotolewa hospitalini hapa.