Contact Us | FAQ | Mails | Complaints |

MASHINE YA KISASA YA MIONZI (Digital x-ray) YAANZA KUFANYA KAZI NDANI YA HOSPITALI YA RUFAA MKOANI NJOMBE.

Posted on: May 23rd, 2020

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe imeanza kutoa huduma za kisasa za uchunguzi wa  mionzi kwa kutumia mashine ya kisasa (Digital x-ray machine) iliyotolewa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na watoto ikiwa ni mkakati wa kuboresha huduma za afya katika hospitali za rufaa za Mikoa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi  huo, Mganga Mfawidhi  Dr.Winfred Kyambile ameishukuru serikali ya awamu ya tano kuona umuhimu wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi kwa kuleta vifaa tiba vya kisasa ili kusaidia upatikanaji wa huduma bora.

Sambamba na hilo Dr.Winfred Kyambile amewakaribisha wananchi wa Mkoa wa Njombe kufika katika hospitali ya rufaa ili  kupata huduma bora za matibabu na vipimo ikiwemo huduma ya uchunguzi wa mionzi.

Kwa upande wake mtaalamu wa mionzi katika Hospitali ya rufaa bwn.Dani Mkama amesema  mtambo huu wa kisasa utasaidia kutoa huduma nzuri kwa jamii kwa sababu una uwezo wa kuhudumia wagonjwa wengi kwa muda mfupi na kutoa picha bora.

Aidha ameahidi kushirikiana vyema na wataalamu wenzake katika kutoa huduma zilizo bora kwa wagonjwa pamoja na kuhimiza kuitunza mashine hii ili idumu katika ubora wake kwa muda mrefu na wananchi waendelee kupata huduma.